Kuhusu Kanisa

Historia Ya Parokia Ya Mtakatifu Petro, Oysteerbay

Parokia Ya Mtakatifu Petro, Oysterbay ipo barabara ya Haile Selasie, mkabala na hoteli ya Protea, katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mwanzo wa Parokia ya Mt. Petro – Oysterbay, unahusishwa na kijiji cha wavuvi kilichokuwa ufukweni mwa bahari ya Hindi, Msasani. Mahali pale palikuwa na mbuyu ambao, chini yake, kilijengwa kikanisa kidogo cha makuti. Kwa sasa kikanisa hicho hakipo tena. Kumbukumbu zinaonesha kwamba kikanisa cha Msasani kilianzishwa miaka ya mwanzoni mwa 1950, wakikadiria 1952. Watu waliopeleka huduma katika kikanisa hicho ni pamoja na Msgr.John Francis Dennis aliyekuwa akitokea katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosef. Kulikwepo na Makatekista waliowatayarisha waamini kwa Sakramenti mbalimbali husan ubatizo, komunyo na kipaimara.

Kutokana na kukua kwa mji na kuongezeka kwa wakazi. idadi ya Wakristo Wakatoliki nayo iliongezeka. Kwa msingi huo waamini waliamua kupanga katika nyumba iliyokuwa kwenye makutano ya barabara za Old Msasani na Karume upande wa kushoto ukitokea baharini. Parokia ya Mt. Petro ilizaliwa hapo na mapadre kutoka Kanisa Kuu la Mt. Yosef walifika hapo kuwapa waamini huduma. Hapa ndipo Msgr. Dennis alianza kazi ya kutayarisha parokia mpya

Katika kitabu chake, ‘Historia ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam’, Msgr. Deogratias Mbiku (Mbiku 1985) anamtaja Padre Franz Solan, Provinciali wa Wakapuchini, kufika pale na kukibariki kikanisa hicho alipokuwa katika ziara yake rasmi (Canonical Visit). Ziara hiyo ilikuwa kiashiria kuwa kikanisa hicho kilikuwa kinajulikana Jimboni na huenda kilikuwa na hadhi ya Kigango.

Mnamo mwaka 1958, Oysterbay ilitangazwa kuwa Parokia kamili. Msgr. John Francis Dennis alikuwa Paroko wa kwanza wa Parokia.

Kwa kuwa nyumba ya Ibada ambamo Parokia ilizaliwa ilikuwa nyumba ya kupanga, halikuwa kanisa la kujitosheleza kwa miundombinu, majengo, vifaa na hata tabaruku mbalimbali za kufanya maadhimisho thabiti ya kikatoliki. Kwa hiyo, Mapadre walikuwa wanaishi bado Katika Kanisa Kuu la Mt. Yosef. Hata maadhimisho ya Sakramenti kama ubatizo, kipaimara na ndoa yalifanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Yosef. Kumbukumbu zinaonesha kwamba muamini wa kwanza aliingizwa katika kitabu cha ubatizo na kipaimara tarehe 17.5.1959; na kuwa waamini wa kwanza kuorodheshwa katika kitabu cha ndoa waliandikishwa tarehe 26.5.1959. Hawa wote walipokea Sakramenti hizo katika Kanisa Kuu la Mt. Yosef.

Hatimaye, Msgr. Dennis alifanikiwa kupata eneo ambapo Kanisa la sasa limejengwa. Awali, eneo hili likuwa mahali pa kuchimba kokoto. Kiwanja kilikuwa na mashimo na miamba. Hatimaye jiwe la msingi wa Kanisa la sasa liliwekwa mwaka 1962. Parokia ya Oysterbay ikawa Parokia kamili yenye Kanisa, nyumba ya mapadre na mapadre wakazi.

Mwaka 2008, Parokia iliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuzaliwa kwake. Parokia ina Kanda 9 moja ikiwa ni maalum kwa waamini wanaosali kwa lugha ya Kiingereza. Kanda hizi zina Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo 57. Aidha, kipo Kigango kimoja cha Mtakatifu Paulo wa Msalaba kilichopo Mikocheni A. Parokia inahudumiwa na Padri mmoja na Parokia ina jumla ya Makatekista 6 wanaotoa huduma za mafundisho ya dini katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo kwenye eneo la mipaka ya Parokia na mafundisho ya matayarisho kwa sakaramenti mbalimbali kwa watoto na watu wazima. Parokia inapata vilevile huduma kutoka kwa Watawa wa kike wa Shirika la Dada Wadogo wa Francisko wa Asizi

Jengo la Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay

Jengo la Kanisa la Mtakatifu Petro - Oysterbay

Kigango cha Mtakatifu Paulo wa Msalaba Mikocheni A

Ratiba ya Misa Kigango cha Mtakatifu Paulo wa Msalaba Mikocheni A:
Misa ya kwanza saa: 1:00 asubuhi
Misa ya pili saa: 2:45 asubhi.

Jengo la Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Paulo wa Msalaba Mikocheni A

Huduma za Jamii zinazosimamiwa na Parokia

Shule ya Chekechea

Parokia inasimamia shule ya chekechea ya Lady Chesham ambayo ni mchepuo wa lugha ya Kiingereza. Shule ipo barabara ya Haile Selasie, mkabala na Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay. Shule imesajiliwa. Shule ina vyumba vya madarasa 4 ambavyo vina uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kwa wakati mmoja. Shule inaongozwa na Mwalimu Mkuu Sister Clementina Mvungi na ina watumishi 14 ambapo kati yao walimu ni 7. Shule inafundisha kwa kutumia mtaala wa Tanzania chini ya Baraza la Mitihani la Taifa kwa kutumia mbinu za ufundishaji na ujifunzaji  za Montesori ikiwa ni pamoja na  kuzingatia taratibu na miongozo yote ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na vilevile yale ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.

Chuo cha Ufundi

Parokia inacho pia Chuo cha Ufundi Stadi kinachotoa mafunzo ya Ushonaji kwa wahitaji mbali mbali. Chuo kinazingatia miongozo ya Baraza la Vyuo vya Ufundi (NACTIVET). Chuo kina bodi na kinaongozwa na Mwalimu Fransisca Tesha.

Miradi

Parokia ina mradi wa Kituo cha Kardinali Rugambwa ambacho kinasimamia jengo lenye ukumbi wa kukodishwa na ofisi za kupanga. Aidha, Kituo vilevile kinasimamia nyumba ya ghorofa yenye nyumba za kupanga iliyopo Kitalu namba 200 Msasani, na Kantini ambayo imekodishwa.

Jengo la Kituo cha Rugambwa social centre

Nyumba ya Kupangisha ya Mtakatifu Petro, Msasani